Karatasi ya maelezo - Ualbino Tanzania
Ualbino ni hali ya kijenetiki inayosababisha ukosefu wa rangi ya asili katika ngozi na nywele, pamoja na uoni hafifu. Ualbino sio ugonjwa na wala hauambukizwi. Mtu mwenye ualbino sio kwamba amelaaniwa na wala sio zimwi, bali ni binadamu. Bila kujali kabila la mtu, mama na baba wasio na ualbino wanaweza kupata mtoto mwenye ualbino.
Watu wengi wenye ualbino Tanzania wanakabiliwa na madhara ya fedheha pamoja na ukandamizwaji kutokana na muonekano wao. Baadhi ya watoto wenye ualbino wanaonewa shuleni, wengine wanatelekezwa na familia zao. Watu wazima wenye ualbino wanaweza kuhangaika kukidhi mahitaji yao kwa sababu hawatakiwi kukaa kwenye jua kutokana na hatari ya kupata kansa ya ngozi. Katika baadhi ya maeneo, watu wenye ualbino wamekuwa wakishambuliwa kikatili, na wengine hata kuuawa.